Vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vimetakiwa kuhakikisha kuwa vinazingatia sheria na taratibu za fedha zinazotolewa na Halmashauri baada kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani wakati wa zoezi la utoaji na urejeshaji wa mikopo.
Rai hiyo imetolewa na afisa maendeleo ya jamii wa manispaa ya Ilemela, Ndugu Sitta Singibala wakati akizungumza na viongozi wa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutoka kata za wilaya hiyo ambapo amewataka kuzingatia utaratibu na sheria ya fedha ya mwaka 2019 inayoratibu zoezi la utoaji wa mikopo kwa vikundi kwa kuhakikisha wanatumia fedha zinazotolewa kwa kufanyia shughuli za kiuchumi zenye tija kwao na zenye kuwawezesha kurejesha mikopo hiyo bila vikwazo na kwa wakati.
“Kazi ya serikali ni kuwawezesha wananchi wake kuishi katika muelekeo sahihi na kupata nafuu ya maisha,mikopo hii ni zoezi endelevu hivyo ni lazima irejeshwe .Leo mmeitwa hapa kwa ajili ya kujaza mikataba na kukumbushwa sheria na taratibu za fedha hizi.Nyie ni viongozi wa vikundi vyenu elimu hii tunayowapatia hapa tunategemea iwafikie wanavikikundi wote.”Amesema.
Nae Afisa Maendeleo ya jamii Bi.Amina Bululu amewataka viongozi hao wa vikundi kuwatumia maafisa watendaji wa kata katika maeneo yao kwa changamoto zozote watakazokumbana nazo katika shughuli zao na wasikimbilie Wilayani kwa kila jambo.
“Watendaji wanao uwezo wa kutatua changamoto nyingi ikiwemo hizi za mikopo ya Halmashauri,una swali uliza kwake ikionekana ni jambo gumu linalohitaji ushiriki wa Maafisa Maendeleo ya jamii sisi tupo kwa ajili yenu”.Amesema.
Aidha Bi Florence Vedasto ambae ni Afisa maendeleo ya jamii mwandamizi ametoa maelekezo ya namna ya kurejesha fedha za mikopo hiyo na kuwataka viongozi wa vikundi kuwa makini katika benki wanayolipia na kutunza kumbukumbu“Ni muhimu kutunza risiti baada ya malipo kwani ndicho kithibitisho pekee kwamba pesa imelipwa.”Amesema.
Akizungumzia sheria ya fedha za mikopo ya mwaka 2019 ,Afisa Vijana wa Halmashauri ya Manispaa Bi.Lucy Matemba amesema endapo kikundi kitashindwa kurejesha kwa wakati sheria hiyo itakutaka ufikishwe mahakamani na ulipe gharama zote za mahakama na hatimae kufanya rejesho chini ya sheria.
“Mikopo hii haina riba ila mnatakiwa kurejesha kama taratibu zinavyowataka mfanye.Hatuna sababu ya kuvutana hadi mahakamani au kutumia nguvu.Sera ya vijana izingatiwe hasahasa kwa vikundi vya vijana.Kama umri umepita jitoe au ubaki kama mshauri wa kikundi.Lengo ni vikundi vya vijana vibaki na uhalisia wake”Amesema.
Kwa kipindi cha kuanzia mwezi July 2019 hadi April 2020 halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imetoa jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 540 kwa vikundi 166 ambapo vikundi 126 ni vya wanawake, vikundi 32 ni vya vijana na vikundi 8 ni vya watu wenye ulemavu, ikiwa ni katika kutekeleza agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya kila mwezi ya Halmashauri kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.