Madiwani wa Manispaa ya Ilemela kupitia mkutano wa Baraza la madiwani wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambalo hupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo katika nyakati tofauti wamepongeza mwenendo mzuri wa Halmashauri.
Hayo yamejiri mara baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri Mhandisi Modest Apolinary kuwasilisha taarifa yake ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha robo ya kwanza, ambapo kwa mujibu wa kanuni za kudumu za halmashauri ya Manispaa ya Ilemela za mwaka 2014, Mkurugenzi anawajibika kulitaarifu baraza la madiwani kwa kutoa taarifa ya matukio mbalimbali ambayo yamefanyika au yanatarajia kutokea katika kipindi cha kila robo mwaka.
Akisoma taarifa hiyo, Mhandisi Modest Apolinary amebainisha kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza Halmashauri imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 5.02 sawa na asilimia 37.1 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2022/2023 ambayo ni mapato ya ndani.
“Halmashauri imefanikiwa kukusanya jumla ya Tshs. 5 , 016,854,151. 61 sawa na asilimia 37.1 ya makisio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo ni mapato ya ndani, jambo ambalo limepelekea kuvuka lengo la makusanyo kwa robo ya kwanza ambalo ilitakiwa kukusanya asilimia 25 hivyo kuvuka asilimia 10 zaidi” Amesema Mhandisi Modest.
Mhandisi Modest ameendelea kufafanua kuwa, kupitia makusanyo ya chanzo cha mapato ya ndani jumla ya Shilingi Milioni 890.28 ziliekezwa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata za Ilemela huku zikigusa sekta za ujenzi ambapo kiasi cha shilingi Milioni 199.99 zilitolewa , Milioni 120.91 zilielekezwa katika sekta ya elimu msingi, Milioni 70.32 sekta ya elimu sekondari, Afya ilipatiwa kiasi cha Shilingi Milioni 100, maendeleo ya jamii Shilingi milioni 194 na Shilingi Milioni 204.3 zilielekezwa sekta ya ardhi.
Ameongeza kusema kuwa, katika kipindi hicho jumla ya maboma 45, ofisi 4 na matundu manne ya vyoo yamewezwa kujengwa katika baadhi ya shule za msingi ikiwa ni jitihada na maono ya Mkuu wa Wilaya huku akitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Ilemela na viongozi wa maeneo hayo kwa jitihada na ushiriki wao katika ujenzi huo.
Wakichangia taarifa hiyo, waheshimiwa madiwani wa kata za Buswelu, Nyasaka, Pasiansi, Nyamhongolo, Buswelu, Kiseke, Nyakato, Kahama Shibula, Bugogwa na Kirumba kwa niaba ya madiwani wengine wamezipongeza jitihada hizo zilizofanyika katika kuiletea maendeleo Ilemela ambapo pongezi nyingi zilielekezwa katika upande wa ukusanyaji mapato na mgawanyo wa mapato hayo ya ndani katika kata zote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kuhusu suala la mapato, Waheshimiwa Madiwani wamempongeza Mkurugenzi, timu ya menejimenti kwa kuweza kushirikiana pamoja kuweza kufikia kiwango hicho cha mapato katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwani ni historia imewekwa huku wakisistiza umoja, uaminifu, mshikamano, uadilifu na usimamizi mzuri ili kuweza kukamilisha miradi viporo katika kata mbalimbali na kuweza kufikia malengo ya Halmashauri.
Pamoja na hayo waheshimiwa madiwani wamemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mkurugenzi pamoja na wataalam kwa maono yao ya uanzishwaji na ushiriki wao katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi kwa kuchimba misingi na kupelekea ukamilishaji wa maboma ya madarasa 45, vyumba 4 vya ofisi za walimu na matundu manne ya vyoo katika kata 10 za Manispaa ya Ilemela.
Akihitimisha Mkutano huo wa Baraza la Madiwani, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amemshukuru Mhe.Rais Samia kwa kuipatia Manispaa yake shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 110 huku akimpongeza Mkurugenzi na timu nzima ya Manispaa hiyo kwa kazi nzuri ya ukusanyaji mapato wanayoendelea nayo na kusisitiza suala la usafi wa mazingira kuwa ni jukumu la wananchi wote wa Ilemela.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.