Katika kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia kitengo cha lishe, imetoa mafunzo kwa wakinamama juu ya swala zima la lishe na utaratibu wa unyonyeshaji kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na zaidi ili kuepuka na maradhi ya utapiamlo na udumavu.
Mafunzo hayo juu ya unyonyeshaji na lishe yalitolewa na afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi Paulina Everest Machango wakati akizungumza na wanawake waliokuja kliniki ya watoto katika zahanati ya Nyerere na kituo cha afya Buzuruga.
Bi Paulina amewataka wakinamama hao kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kunyonyesha maziwa ya mama pekee bila aina nyingine yeyote ya chakula kwa watoto wa chini ya miezi sita ili kuwakinga watoto hao dhidi ya magonjwa ya utapiamlo na udumavu huku akisisitiza kuhakikisha wanawapatia mlo kamili watoto wote wenye umri wa zaidi ya miaka miwili ili waweze kuwa na afya njema na imara
“Wamama wengi tuna watoto wenye utapiamlo ule wa kati kitu ambacho ni hatari maana tukizembea kidogo wanaanza kuugua wanalazwa, na hii yote ni kwasababu ya unyonyeshaji na ulishaji, usiofaa kwa mtoto” ,Alisema
Aidha Bi Paulina alikemea mila potofu na tabia zisizofaa zinazochangia udumavu kwa watoto ikiwemo kuwazuia kula baadhi ya vyakula muhimu na utandawazi mbovu kwa wakinamama wa kuogopa kunyonyesha inavyotakiwa watoto wao wakikwepa kudondoka kwa maziwa katika vifua vyao.
Kwa upande wake muuguzi wa kituo cha afya Buzuruga Bi Grace Msabaha ametaja faida mbalimbali zinazopatikana kwa kufuata utaratibu mzuri wa unyonyeshaji ikiwemo kupata mtoto mwenye afya na kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo utapiamlo, kuimarisha mahusiano baina ya mtoto na mzazi pamoja na kutumika kama njia ya uzazi wa mpango kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo katika ukuaji wa mtoto.
Bi Sarafina Isaac ni mmoja ya mama aliyehudhuria kliniki ya elimu ya unyonyeshaji na lishe anaeishi mtaa wa Buzuruga, ameshukuru kwa elimu iliyotolewa na wataalamu hao huku akiwasihi wamama wenzake kuzingatia utaratibu wa kunyonyesha na lishe kwa watoto ili kujenga kizazi kilichokuwa salama na chenye afya bora katika jamii.
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 ya mwezi wa nane yakiwa na lengo la kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama na pia kuweka msukumo wa kipekee katika kuunganisha nguvu ya wadau mbalimbali ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Kwa mwaka 2020 maadhimisho haya yalibeba kauli mbiu ya "Tuwawezeshe Wanawake Kunyonyesha kwa Afya Bora na Ulinzi wa Mazingira"
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.