Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wataalam kutoka mradi wa PS3 pamoja na OR-TAMISEMI imekamilisha zoezi la ufungaji wa mfumo wa GOTHOMIS katika vituo vyote vya afya vitatu pamoja na zahanati zote 13 zilizopo katika Manispaa ya Ilemela.
Mfumo huu utakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa pindi watakaposajiliwa kwa mara ya kwanza mapokezi, anapokwenda kumuona daktari, maabara, dirisha la dawa, lakini pia utakuwa na uwezo wa kutambua wagonjwa wa msamaha na kuweza kupata huduma stahili.
Afisa Tehama wa Manispaa ya Ilemela Bi Faraja Ndaro Ezekiel amesema kuwa mfumo huu utakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa pindi wanaposajiliwa kwa mara ya kwanza mapokezi, anapokwenda kumuona daktari, maabara, dirisha la dawa, lakini pia utakuwa na uwezo wa kutambua wagonjwa wa msamaha na kuweza kupata huduma stahili huku akiwaasa watoa huduma hao kuhakikisha wanautumia mfumo huo. Pia amewataka watoa huduma za afya kuwasiliana na Kitengo cha Tehama pindi zinapojitokeza changamoto za kitaalamu ili kupata msaada badala ya kutumia utaratibu wa zamani wa kuandika kwenye makaratasi.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Daktari Florian Tinuga amewataka watoa huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya vya halmashauri ya manispaa ya Ilemela kusimamia na kuutumia mfumo huo wa kielektroni pindi wanapohudumia wananchi na pia kuhakikisha wanaivitunza vifaa hivyo.
Nae mteknolojia maabara ya kituo cha afya Buzuruga Bwana Valentino Mayunga amesema kuwa tangu kuanza kuutumia mfumo huo umemsaidia kurahisisha kutoa huduma kwa haraka kwa kutuma majibu kwenda kwa daktari, kuwa na taarifa sahihi za wagonjwa na kuandaa kwa urahisi taarifa za mwisho wa mwezi.
Nae Bi Salome Masanja aliefuata huduma kituoni hapo ameusifu utaratibu wa kutumia mfumo wa kielektroniki katika kutoa huduma kwani unasaidia kupunguza msongamano kwa wagonjwa hivyo kupata huduma kwa wakati tofauti na zamani ambapo mgonjwa alikuwa anatumia muda mrefu kwenye foleni kwa kuzunguka kutoka sehemu moja ya huduma kwenda nyingine bila utaratibu mzuri .
GOTHOMIS ni mfumo ulioandaliwa na wataalamu wa OR-TAMISEMI kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa na kuratibu shughuli nzima za hospitali ikiwemo kudhibiti upotevu wa mapato.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.