Mhe Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameipongeza Manispaa ya Ilemela kwa kuendelea kupata hati safi kwa mara ya tano mfululizo, huku akiitaka manispaa hii kuhakikisha haizalishi hoja mpya za ukaguzi kwa kuzijibu kwa wakati, ili ziweze kufungwa.
Ameyasema hayo mbele ya mkutano wa baraza la madiwani ulioketi tarehe 17 juni 2025 kwa ajili ya kupokea na kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na utekelezaji wake.
"Tuendelee kuhakikisha hatuzalishi hoja mpya za ukaguzi kwa kujibu kwa wakati, na zifungwe ili tusizalishe hoja mpya, pamoja na kutekeleza kikamilifu maoni ambayo yanatolewa na CAG sambamba na kushirikiana nae ili kuendelea kuzipatia majibu hoja hizo"
Aidha Mhe Mtanda amesisitiza juu ya ushiriki wa idara zote kikamilifu wakati wa kujibu hoja hizo zinapojitokeza, "hii ni halmashauri na sio kampuni ya mtu binafsi idara zote ni lazima zishirikishwe pale hoja zinapojitokeza", amesisitiza.
Akiwasilisha majibu ya ukaguzi huo, Ndugu Richson Ringo ambae ni mkaguzi mkuu wa nje wa mkoa wa Mwanza amesema kuwa katika mwaka 2023/2024 manispaa ya Ilemela ilipata hati safi (unqualified opinion).
Aidha ndugu Ringo amesema kuwa sababu iliyopelekea hoja au mapendekezo yaliyosalia kutokufungwa inatokana na kukosekana kwa mikakati thabiti na ya dhati kwa watekelezaji pia kutokushirikishwa ipasavyo kwa wakuu wa idara wanaohusika na hoja hizo, sambamba na majibu ya menejimenti yanakosa vielelezo na ushahidi wa kutosha ili kuwezesha kufungwa kwa hoja hizo.
Mariam Mshana, ni mweka hazina wa manispaa ya Ilemela akiwasilisha taarifa ya hoja zilizojitokeza kwa niaba ya mkurugenzi amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri ya manispaa ya Ilemela ilikutwa na hoja 42 ambapo hadi sasa hoja 30 zimefungwa na hivyo kubakiwa na hoja 12 ambazo zipo katika utekelezaji ikiwa ni sawa na asilimia 71 ya hoja ambazo zimefungwa .
Vilevile, Bi Mariam amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano (5) mfululizo kuanzia mwaka 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 halmashauri ya manispaa ya ilemela imeendelea kupata hati safi na kubainisha kuwa sababu iliyopelekea kupata hati hiyo ni ushirikiano baina ya wataalam, waheshimiwa madiwani, ofisi ya mkuu wa wilaya na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kuhakikisha halmashauri inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Nae mbunge wa jimbo la Ilemela, Mhe Dkt Angeline Mabula amepongeza kwa kazi nzuri inayoendelea kutekelezwa na watendaji wa ilemela chini ya mkurugenzi, huku akihoji juu ya hoja nne ambazo zipo katika utekelezaji na hazijafungwa ambapo alitumia fursa hiyo kumuomba mkuu wa mkoa kutatua juu ya suala la hoja ya ardhi kuuzwa na jiji la mwanza ikiwa ipo kwenye ardhi ya manispaa ya ilemela pasipo kuishirikisha manispaa ya ilemela.
Kila baada ya mwaka wa fedha kuisha, halmashauri zinapaswa kuwasilisha taarifa zake za hesabu kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa ajili ya ukaguzi na baada ya kufanyiwa ukaguzi, halmashauri hupewa nafasi ya kujibu hoja zake na ukaguzi huu hufanyika kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa (Local Government Finance Act, 1982), iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.