Jamii imetakiwa kuwa na mtazamo chanya dhidi ya mpango wa elimu ya msingi kwa watoto walioikosa MEMKWA ili kutoa fursa ya wanafunzi wasiokuwa katika mpango wa kawaida kunufaika na programu hiyo.
Rai hiyo imetolewa na mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa elimu msingi wa manispaa hiyo Mwalimu Mashelo Bahame ambapo amefafanua kuwa zipo changamoto mbalimbali zinazosababisha watoto kukosa elimu lakini Serikali kwa kutambua hilo imeweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu japo jamii wakati mwengine inazidharau na kuzikejeli juhudi hizo.
'.. Zamani kulikuwa na makundi matatu yanayosimamia elimu kwa watoto wetu, jamii, walezi wakiwemo walimu na wazazi, Lakini siku hizi jamii imejitenga na jukumu hili na kundi la wazazi limejitenga pia wako na mambo mengine, Watoto wanalelewa na wafanyakazi wa ndani na luninga na haya mambo ya elimu wanayabeza hayana umuhimu kwao ..' Alisema
Aidha Mwalimu Mashelo amelipongeza shirika la SOS kwa utekelezaji wa miradi ya elimu pamoja na kuwalea watoto waishio katika mazingira magumu ndani ya manispaa yake na mkoa wa Mwanza kiujumla huku akiwashukuru viongozi wa wilaya ya Ilemela Mkurugenzi Bi Ummy Mohamed Wayayu, Mbunge Dkt Angeline Mabula na kiongozi mkuu wa wilaya hiyo Mwalimu Hasan Elias Masala kwa juhudi zao katika kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya elimu .
Kwa upande wake afisa elimu watu wazima manispaa ya Ilemela Mwalimu Recipius Masatu Magembe amesema kuwa mpango wa kutoa elimu kwa walioikosa MEMKWA ulianza mwaka 1999 hadi 2022 kwa majaribio katika wilaya za Kisarawe, Songea vijijini, Masasi, Musoma vijijini na Ngara na baada ya mpango kuonekana unafaa mwaka 2003 Serikali ikauingiza mpango huo katika shule zote nchini ili kuwasaidia watoto wote waliokosa elimu na Kwa wilaya ya Ilemela mpaka sasa zaidi ya watoto 1060 wamesajiliwa na wamekuwa wakifanya vizuri sanjari na kukemea dhana potofu ya kuamini elimu za nje ya darasa au kujiendeleza hazina manufaa yeyote .
Celestine Mwalongo ni mratibu wa miradi ya elimu katika shirika la SOS ambapo ameishukuru manispaa ya Ilemela kwa ushirikiano wake katika kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu inayofanywa na shirika lake huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazokabili sekta ya elimu .
Nae Mwalimu Sara Loom kutoka kabangaja shule ya msingi na Beatrice Magesa kutoka Kahama shule ya msingi kwa pamoja wameshukuru uwepo wa mafunzo hayo kwani yamewaongezea ubunifu katika kuwasaidia watoto wa awali na wanaoupata elimu nje ya mfumo wa kawaida.
Mafunzo kwa walimu na waratibu wa elimu kata yamefanyika kwa siku mbili kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la SOS ambapo lengo kuu ni kuwaongezea maarifa na ujuzi walimu kuweza kusimamia vizuri elimu katika maeneo yao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.