Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ya Manispaa ya Ilemela imewataka wahudumu wa afya kutoa huduma nzuri na za viwango vinavyotakiwa kwa wateja wao hayo yamesemwa wakati wa ziara ya kukagua zahanati zinazotoa huduma na ushauri nasaha kwa walioathirika na ugonjwa wa UKIMWI.
Katika ziara hiyo, kamati hiyo ilipokea taarifa za zahanati hizo za Ilemela,Pasiansi na Buswelu zilizoainisha huduma zinazotolewa ikiwemo ushauri nasaha na kupima VVU,huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,huduma ya uangalizi na matibabu ya kufubaza maambukizi ya VVU sambamba na kuzalisha kina mama wajawazito.
Aidha taarifa hiyo ilitaja mafanikio katika huduma za UKIMWI zinatolewa ikiwemo ongezeko la madawa na vitenganishi kutoka serikalini na wadau wa ICAP wanaojishughulisha na masuala mbalimbali ya afya ikiwemo UKIMWI.Kuweza kutoa huduma za mkoba na kuweza kuibua watu wapya wenye maambukizi na kuwapa huduma stahiki.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.Sadick Manusura akiwaongoza wajumbe wa kamati hiyo amesema kuwa jamii nzima inao wajibu wa kuwajali waathirika na kuungana katika kuboresha huduma za UKIMWI huku akikiri kuzitambua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi.
“ Jamii nzima tunaowajibu wa kuwajali watu hawa kwa kuungana katika maboresho ya huduma za UKIMWI tukianza na kuboresha na kujenga vituo bora vya kutolewa huduma hizi maalum kwa wenzetu walioathirika kwa kutambua kuwa janga hili ni letu sote ”. Amesema Mhe.Manusura
Daktari Samson Marwa ambae ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela ameiasa jamii ya Ilemela kuacha kufanya ngono zembe kwani ndio njia kuu ya kupata maambukizi ya VVU.
“ Zipo njia nyingi za kupata maambukizi, kutumia pamoja vitu vyenye ncha kali vilivyotumiwa na mtu mwenye maambukizi,mtoto kupata maambukizi wakati wa kuzaliwa lakini njia kubwa kabisa ni kufanya ngono zembe. Hivyo tuache ” Amesema Dkt.Marwa.
Nae Mhe. Juma Wesa mjumbe wa kamati hiyo amesisitiza elimu ya UKIMWI iendelee kutolewa kwa makundi mbalimbali ndani ya Manispaa ya Ilemela ikiwemo makundi ya wanaotumia madawa ya kulevya kwani hata wao ni rahisi kupata maambukizi na kushindwa kujimudu kimaisha wakiachwa na upweke.
Baadhi ya wagonjwa wa VVU wanaohudhuria kliniki katika zahanati hizo wamefurahishwa na utaratibu huo wa Manispaa ya Ilemela kutembelea na kufuatilia kwa karibu huduma za UKIMWI zinavyotolewa na kuendelea kupambana na changamoto zilizopo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.