Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia changamoto za kina mama na watoto wa kike Kivulini jijini Mwanza limeunga mkono juhudi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika kupambana na janga la korona linaloitikisa dunia kwa sasa kwa kukabidhi vifaa muhimu vinavyotumika katika kujilinda na kujikinga na gonjwa hilo.
Akizungumza katika ukumbi wa manispaa ya Ilemela wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ndugu Yassin Ally amesema shirika la Kivulini ni wadau wa maendeleo wa muda mrefu na wamefanya kazi nzuri na manispaa ya Ilemela katika shughuli zao za kutetea haki za kina mama na watoto wa kike katika jamii nchini Tanzania.
“Hatuna budi kuungana na juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya janga hili.Tunafahamu kuwa serikali ilichukua maamuzi ya kufunga shule ili kuwalinda watoto kutoka kwenye misongamano ambayo ni njia rahisi ya kupata maambukizi ya Korona,jamii ichukue tahadhali zaidi katika kuwalinda watoto na mimba za utotoni na manyanyaso ya aina yoyote yanayoweza kujitokeza kwa kipindi hiki.”
Ndugu Sitta Singibala kwa niaba ya Mkurugenzi alisema kuwa, mbali na kuahidi kusimamia vyema msaada uliotolewa amewashukuru Kivulini kwa kujitoa kwao kwa jamii ya Ilemela na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika shughuli zao za kutetea haki na kupambana na changamoto mbalimbali za kina mama na watoto wa kike.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na barakoa boksi 3,vitakasa mikono chupa 51,vipima joto 6 na sabuni chupa 17 vitakavyogawiwa na kutumika katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.