Zoezi la kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero, malalamiko, changamoto na utoaji wa elimu juu masuala ya ardhi na ulipaji wa kodi zake maarufu kliniki za ardhi umesaidia kupunguza mlundikano wa wananchi katika ofisi za ardhi za wilaya ya Ilemela na mkoa wa Mwanza kwa ujumla
Hayo yamesemwa na kamishna wa ardhi msaidizi mkoa wa Mwanza Bi Happines Mtutwa wakati wa zoezi hilo katika ofisi za kata ya Pasiansi ambapo amefafanua kuwa zoezi la kliniki ya ardhi ni endelevu na limekuwa na manufaa makubwa siku hadi siku huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano
'.. Zoezi limeendelea kuwa la mafanikio makubwa sana, Hata ule mrundikano wa watu kwenye maofisi yetu umepungua sana, Zamani ilikuwa ukifika ofisini kwetu hata pale ofisi za ardhi manispaa ya Ilemela ilikuwa unakuta watu wengi sana kama tupo kariakoo lakini siku hizi hauwezi kuliona hilo ..' Alisema
Aidha Bi Mtutwa ameongeza kuwa changamoto kubwa iliyosalia kwa sasa ni kero ya fidia ambayo nayo imeendelea kufanyiwa kazi na wakurugenzi wa halmashauri kwa kutenga fedha kwa awamu na kulipa wananchi waliotwaliwa maeneo yao na Serikali kwaajili ya shughuli mbalimbali za kijamii
Kwa upande wake afisa maendeleo ya ardhi manispaa ya Ilemela Bi Grace Isaac Masawe amesema kuwa wamesogeza huduma za ardhi karibu ya wananchi ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma kwa kuwa wapo wengine wagonjwa hawawezi kwenda maeneo ya mbali, wengine ni wazee na wengine ni masikini hawawezi kumudu gharama za kufata huduma ofisi za manispaa hivyo kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na sahihi katika umbali mfupi na kwamba zaidi ya hati thelathini zimetolewa kwa wananchi wa kata ya Pasiansi sanjari na kuwaomba wananchi kujitokeza katika maeneo yao wanaposikia matangazo ya uwepo wa kliniki za ardhi
Mheshimiwa Rosemary Onesmo Mayunga ni diwani wa kata ya Pasiansi ambapo ameishukuru na kuipongeza Serikali kupitia wizara ya ardhi na wataalam wa ardhi manispaa ya Ilemela kwa kuweka utaratibu wa kufika katika maeneo ya wananchi na kutatua kero za wananchi kwani imeongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao kwa kuwa wengi walikuwa wameshakata tamaaa baada ya kufuatilia huduma za ardhi kwa muda mrefu huku akiomba zoezi hilo kuwa endelevu
Nae mkazi wa Lumala Bi Eva Sylvester Agila amesema kuwa hatua ya ugawaji wa hati maeneo karibu na wananchi ni sahihi kwa wakati tulionao kwani hapo awali ilikuwa unafuatilia hati kwa muda mrefu na gharama kubwa za usafiri kufika ofisi za ardhi huku faida kubwa ya hati miliki ikiwa ni kuongeza thamani ya ardhi
Jumla ya hati thelathini zimekabidhiwa kwa wananchi wa kata ya Pasiansi na kamishina wa ardhi msaidizi mkoa wa Mwanza na kusikiliza kero na migogoro ya ardhi kwa wananchi sambamba na kutoa elimu ya masuala ya ardhi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.