Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mheshimiwa Daktari Severine Lalika amewataka maafisa elimu kata kuzitumia pikipiki kwa kazi iliyokusudiwa.
Ametoa maelekezo hayo alipokuwa akikabidhi jumla ya pikipiki kumi na tisa kwa maafisa elimu kata wa kata zote 19 za Manispaa ya Ilemela zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Daktari John Magufuli.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mheshimiwa Lalika amemshukuru mheshimiwa Rais Daktari John Magufuli kwa kuleta pikipiki hizo zitakazosaidia kurahisisha utendaji kazi kwa maafisa elimu kata ili kunyanyua kiwango cha ufaulu na kusisitiza kuwa Serikali itakuwa makini kufuatilia matumizi sahihi ya pikipiki hizo.
‘… Nipende kuwaasa tu kuwa Serikali tuliyonayo ni makini hivyo ni lazima itakuwa inafuatilia matumizi ya vifaa hivi ambavyo vimeletwa kaajili ya manufaa ya watu wote wanaotegemea kupata huduma yenu …’ Alisisitiza
Aidha Mkuu wa Wilaya amemtaka Mkurugenzi kuhakikisha kuwa maafisa elimu kata ambao hawana elimu ya vyombo vya moto wanapata mafunzo hayo ili kuepuka ajali na uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga amebainisha matarajio yake kutoka kwa maafisa hao baada ya kukabidhiwa nyenzo hizo ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya usimamizi wa elimu, ufuatiliaji wa elimu na kuongezeka kwa ufaulu huku akisisitiza kuwa watendaji wote waliokabidhiwa vyombo hivyo wanaowajibu wa kuvitunza, kuvilinda na kuvitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria watendaji wote watakaovitumia isivyostahili.
Sambasamba na hayo, Ndugu John Wanga alisema kuwa anaendelea kutambua juhudi za Mhe. Mbunge wa jimbo la Ilemela Angeline Mabula kwa mchango wake katika kusaidia kuinua sekta ya elimu pamoja na sekta zingine jimboni.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela mheshimiwa Renatus Mulunga amewaasa watendaji hao kuwa waadilifu katika shughuli zao za kila siku ili kuinua taaluma wilayani humo kwani mafanikio yatakayopatikana hayatakuwa ya mtu mmoja isipokuwa ya jamii kwa ujumla wake.
Kwa niaba ya maafisa elimu kata, Mwalimu Lucas Mlesi ambae pia ni afisa elimu kata ya Pasiansi alihitimisha zoezi hilo kwa kuishukuru Serikali kwa kutoa pikipiki hizo huku akiahidi kuzitunza na kuzitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.