MFUMO WA UHASIBU NA UTOAJI WA TAARIFA ZA FEDHA KUSAIDIA UDHIBITI WA FEDHA ZA UMMA
Mfumo wa Uhasibu na Utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma unaojulikana kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) utasaidia udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha za Umma sanjari na kuongeza Uwazi na Uwajibikaji kwa vituo vya kutolea huduma za wananchi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Ndugu Omary Kamatta alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji hilo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa uhasibu na utoaji wa taarifa katika vituo vya kutolea huduma yanayotolewa na mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma ujulikanao kama Public Sector System Strengthening (PS3) kwa wataalamu wa vituo vya afya na waratibu Elimu kutoka wilaya za Ilemela na Nyamagana kwa ufadhili wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI ikishirikiana na shirika la maendeleo ya kimataifa la Marekani (USAID)
“Zipo changamoto za upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali fedha zilizopo katika vituo vyetu vya huduma na hivyo halmashauri kushindwa kutoa taarifa sahihi za matumizi ya ruzuku zinazotolewa katika vituo hivyo wakati mwingine kusababisha halmashauri husika kupata hati ya mashaka kutoka kwa mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG). Hivyo Mfumo huu sasa utasaidia kuhifadhi taarifa za mapato na matumizi kunakoongeza uwazi na uwajibikaji wa vituo hivi”, Alisema
Akitoa maelezo ya awali Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Mradi wa Uimarishaji mifumo ya sekta za Umma (PS3) Bi Leah Mwainyekule amesema kuanzia Julai 1, 2017 Serikali inataraji kuanza kupeleka rasilimali fedha moja kwa moja kwenye vituo vya afya na sekta ya elimu kwa ngazi ya halmashauri hivyo mafunzo walioanza kuyatoa kwa ngazi ya taifa, halmashauri na kwa watumiaji wa mwisho katika mikoa Ishirini na Sita ya Tanzania Bara yanalenga kusaidia kuongeza uelewa mpana na maarifa ya stadi za kuwezesha utendaji wa moja kwa moja kwa watumishi waliochaguliwa katika kituo kukabiliana na changamoto za utunzaji wa taarifa za fedha zinazowakabili
Aliongeza kwa kusema kuwa, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), wametoa mafunzo ya kina kwa wakufunzi 490 katika ngazi ya taifa na halmashauri nchini kote. Mafunzo hayo yalifanyika katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mtwara, na Shinyanga, ambao nao sasa wanajukumu kuwawezesha watumishi katika vituo vya Sekta ya Afya na Elimu kupata ujuzi wa namna ya kutumia mfumo mpya wa FFARS.
Mfumo huo wa FFARS ambao unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID una lengo la kuongeza ufanisi, hususan katika masuala mazima ya mapato, na ndio utakuwa mtatuzi wa malalamiko ya wananchi.
Akihitimisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela mbali na kuishukuru PSE kwa utoaji wa mafunzo amewaasa wataalamu waliohudhuria mafunzo hayo kuzingatia elimu wanayopewa ili kuongeza ufanisi katika kutimiza majukumu yao
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.