Na Violencea Mbakile-Ilemela
Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha inasimamia suala zima la ukusanyaji wa mapato katika stendi ya mabasi na eneo la maegesho ya malori Nyamhongolo kwa kuweka mifumo bora ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato.
Mhe. Dkt Mpango ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa stendi hiyo mapema tarehe 13 septemba 2022 na kuitaka Ilemela kuwa mfano mzuri wa kuigwa wa ukusanyaji wa mapato katika stendi hii.
“Nataka Ilemela muwe ni mfano wa kuigwa wa kukusanya mapato katika kituo hiki , hakikisheni mnasimamia na kuweka mifumo bora ya kielektroniki ya ukusanyaji mapatio yanayotokana na kituo hiki, nisingependa kuona mapato yanapotea hivyo mianya yote ya upotevu wa mapato izibwe kabisa ”. Amesisitiza
Pamoja na hayo amehimiza kuwa anataka kuona mabadiliko katika suala zima la mapato ya Ilemela kufuatia ujenzi wa kituo hiki kwani kituo hiki ni fursa kubwa hivyo anatarajia kuona makusanyo yanaongezeka mara dufu na kuelekeza ufanyike usimamizi mzuri wa kituo.
Aidha amewataka wananchi kuchangamkia fursa za biashara na ajira zilizopo katika kituo hiki pamoja na kuhakikisha kuwa wanakitunza na kuendelea kuwa safi ili kiweze kudumu.
Nae Mbunge wa Ilemela na Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi, Mhe Dkt Angeline Mabula pamoja na kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ametumia fursa hiyo kuwasilisha kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ilemela cha uhaba wa maji nakumuomba Makamu wa Rais kumsaidia kuiondoa kero hiyo ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Ilemela.
Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI awali akimkaribisha Makamu wa Rais, amemshukuru kwa kuridhia kufungua stendi hiyo na kumuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa huku akimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kubainisha kuwa kupitia Serikali ya awamu ya sita Ilemela itanufaika na miradi wa kimkakati ambayo itahusisha ujenzi wa soko la Kirumba na barabara zinazonguka soko hilo, ujenzi wa Barabara za Buswelu-Busenga hadi CocaCola, na Ujenzi wa barabara ya Buswelu, Nyamadoke hadi Nyamhongolo ambapo miradi hii yote itagharimu kiasi cha fedha za kitanzania takriban Shilingi bilioni 28.8.
Mhe. Dkt Mpango, akihitimisha ametoa maagizo mbalimbali kwa uongozi wa Manispaa ya Ilemela, yakiwemo na kuhakikisha kuwa stendi inakuwa na majokofu ya kutunzia bidhaa zinazoharibika kwa kipindi kifupi, kuhakikisha ujenzi wa jengo la machinga unaanza mara moja pamoja na kuhakikisha Manispaa ya Ilemela inaondoa kero ya vumbi na tope katika eneo la stendi ya daladala ikiwa ni pamoja na kupendezesha stendi kwa kupanda miti
Mradi wa Ujenzi wa stendi ya mabasi na eneo la maegesho ya malori Nyamhongolo hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 26. 6 fedha za kitanzania ambao umejengwa na mkandarasi STECOL CORPORATION kampuni kutoka China, chini ya mtaalam mshauri (BICO) kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.