John Wanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ameitaka Idara ya elimu kuhakikisha vifaa vya watoto wenye mahitaji maalum vinawafikia wahusika waliokusudiwa pamoja na kutoa miongozo ya namna ya kuvitumia na kuvitunza ili vikawe msaada kwa kundi husika.
Ameyasema hayo alipokuwa akipokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto wa Ilemela wenye mahitaji maalum kutoka serikali kuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aidha alisisitiza kuwa ni jukumu la jamii nzima kila mmoja kwa nafasi yake kuwapenda na kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanakuwa salama na kupata mahitaji yao yote ya msingi kwa wakati.
Pamoja na hayo ameishukuru serikali ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonyesha upendo na kuguswa kwa namna tofauti katika kuwatetea na kuona umuhimu wa kundi hili maalum ndani ya jamii yetu.
Makundi ya wanafunzi hao wenye mahitaji maalum ni pamoja na wanafunzi wenye ulemavu wa akili na usonji, viziwi, wasio ona, albino pamoja na wenye ulemavu wa viungo vya mwili waliopo katika shule za msingi za serikali zenye mahitaji maalum katika Manispaa ya Ilemela ambazo ni Ibeshi, Kayenze, Buswelu, Nyamanoro, Sabasaba, Kirumba na Pasiansi
Jumla ya Vifaa 338 vilivyopokelewa ni pamoja na vifaa vya kufundishia kuandika na kusoma ‘alphabet training plate’, vifaa vya kuandikia kwa ajili ya wasio ona, miwani ya kupunguza mionzi ya jua , kengele pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya michezo.
Vifaa hivi vimelenga kuhakikisha watoto wote wakitanzania wanapata elimu iliyokusudiwa ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa sera ya Elimu ya mwaka 2014 inatekelezwa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.