Mhandisi Modest Apolinary, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ameutaka uongozi wa Kata ya Bugogwa kuhakikisha ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari ya Igogwe unaanza mara moja huku akisisitiza kuhusu suala la mafundi na vibarua watakaohusika na ujenzi huo kutoka ndani ya kata ya Bugogwa.
“Tungependa mafundi na vibarua watoke hapa tusije kukuta fundi au vibarua wanatoka mjini wote watoke katika mazingira haya ili hizi fedha zote zibaki kwenye kata hii ni imani yangu baada ya kukamilika kwa ujenzi huu vijana wetu watakuwa wameshapata mitaji ya kuendelea na biashara zao kwasababu hizi fedha tungependa zibaki hapahapa”, Amesema Mhandisi Apolinary
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa utekelezaji wa program ya mpango wa kupunguza umaskini (TPRP- IV) kupitia mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Manispaa ya Ilemela.
Aidha alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Afisa elimu Sekondari kuhakikisha kuwa vyoo katika shule hiyo vinakamilika ndani ya wiki mbili ili watoto waanze kutumia miundominu ya madarasa manne yaliyopo katika shule ya sekondari ya Igogwe yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kata ya Bugogwa huku ujenzi wa miundombinu mingine ukiendelea
Nae mratibu wa TASAF- Ilemela Ndugu Frank Ngitao alibainisha kuwa Ilemela imeshapokea kiasi cha shilingi Milion 308.56 ikiwa ni awamu ya kwanza kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi iliyoombewa fedha ambapo alisema kuwa fedha hiyo itatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika shule ya sekondari Bugogwa ambapo itatekelezwa na mitaa mitano ya Kata ya Bugogwa.
Aliongeza kusema kuwa utekelezaji wa miradi hii utafanywa na jamii kupitia kamati za usimamizi wa shughuli za TASAF katika mitaa husika chini ya usimamizi wa wataalam wa Ilemela na sekta husika kwa kuzingatia miongozo ya TASAF huku akisema kuwa miradi hii inatakiwa kukamilishwa katika kipindi cha miezi mitatu, kuanzia mwezi Aprili hadi Julai 2022.
Nae Diwani wa Kata ya Bugogwa Mhe. William Mashamba pamoja na kuishukuru serikali kwa mradi huu amewataka wananchi wa kata hiyo Kila mmoja kuwa askari wa mwenzake huu kwani huu ni mradi ni wao, huku akiwahimiza vijana kufanya kazi kwa bidi kwani kupitia mradi huu wamepata ajira.
Wananchi wa Kata Bugogwa hususana mitaa ya Nkoloto, Masemele B, Igogwe A, Bugolanya na Isanzu ambao watatekeleza awamu ya kwanza ya mradi wameishukuru serikali kwa kuwajali huku wakiomba changamoto za nyumba za walimu kutatuliwa ili walimu waweze kuishi maeneo jirani na shule.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni kati ya Halmashauri 33 nchini zinazotekeleza mradi wa kupunguza umaskini awamu ya nne kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ambao utajumuisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya afya , elimu na maji, miradi ya ajira za muda pamoja na miradi ya kukuza kipato cha kaya.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.