“Namshukuru Mhe.Rais kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya yetu ya Ilemela ambapo zaidi ya shilingi bilioni 7 zimeshatumika kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya.”
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hasan Masala alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ambapo alitumia nafasi hiyo kufafanua masuala mbalimbali yanayoendelea katika Wilaya ya Ilemela.
Mhe. Masala alitumia pia nafasi hiyo kuwatoa wananchi wasiwasi juu ya zoezi linaloendelea la uandikishaji wa anwani za makazi kwani hili ni zoezi la kitaifa lililotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia S.Hassan na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watendaji wanaofanya kazi hiyo.
“Nitoe rai kwa wananchi wote wa Ilemela kutoa ushirikiano kwa wataalam wanaoendelea na zoezi la anwani za makazi huko mitaani kwetu,nafahamu zoezi hili linahusisha kuandika namba katika majengo mbalimbali yaliyopo mitaani kwetu,majengo ya makazi,biashara na maeneo yaliyo wazi.Wananchi msiwe na wasiwasi hili ni zoezi la kitaifa lililotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia S.Hassan.”
Aliongeza kusema kuwa Wilaya ya Ilemela imetenga siku 40 kukamilisha zoezi hili kwa kuhakikisha wananchi wote wa Ilemela wamepata namba za kuwatambulisha na baadae kuwasajiri katika mfumo wa anwani za makazi utakaowawezesha kutambulika na kuonekana duniani kote.
Mhe. Hasan Masala alihitimisha kwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kilele cha kampeni ya usafi katika mkoa wa Mwanza ambayo ilizinduliwa na Mhe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ambapo kilele kitafanyika siku ya tarehe 26/02/2022 katika Manispaa ya Ilemela kata ya Kirumba eneo la Mwaloni.
“Nahamasisha wananchi wote wa Ilemela kushiriki kampeni ya usafi wa mazingira iliyozinduliwa na mkuu wetu wa mkoa Mhandisi Robert Gabriel,natambua wana Ilemela usafi ni jadi yetu,kilele cha kampeni hii ni Februari 26 mwaka huu na usafi uendelee siku zote usiishie siku ya kilele.”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.