Takriban kiasi cha shilingi bilioni 21.52 zimepokelewa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Ilemela, hayo yamebainishwa katika taarifa ya utendaji kazi na uwajibikaji katika mwaka wa fedha 2022/2023
Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ndugu Herbert Bilia ambae ni mchumi wa Manispaa ya Ilemela amefafanua kuwa fedha hizo ni kutoka Serikali Kuu, Wadau wa maendeleo, Program na Mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi Bilioni 11.63 zilipokelewa kutoka serikali kuu na kutumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa shule mpya, ununuzi wa vifaa tiba, ukamilishaji wa ujenzi vyumba vya maabara, elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa zahanati mpya, na ujenzi wa bweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.
Sambamba na fedha hizo kiasi cha Shilingi 83.76 zilipokelewa kutoka serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa mfuko wa jimbo ambapo zimetumika kukarabati barabara za mitaa, ujenzi wa nyumba ya mtumishi, utengenezaji wa madawati,uwekaji umeme na maji katika shule za msingi na sekondari, ununuzi wa pikipiki na ununuzi wa saruji 100 kwa jili ya ujenzi wa kituo cha polisi.
Shilingi Bilioni 8.7 ni fedha kutoka chanzo cha mapato ya ndani ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya Afya, Elimu, uvuvi, upimaji wa ardhi, maendeleo ya jamii, barabara, masoko na biashara.
Baadhi ya miradi ambayo imetekelezwa na fedha hizo za mapato ya ndani,katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 ni pamoja na kiasi cha Shilingi milioni 479 zimekopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Shilingi Bilioni 5.89 zimetumika kulipa fidia ya ardhi na sehemu ya deni la ardhi, ununuzi wa mashine za POS kwa ajili ya mfumo mpya wa TAUSI, uwezeshaji wa ujenzi wa ofisi za mtaa na kata, matundu ya vyoo , ukamilishaji wa maboma.ununuzi wa madawati kwa shule za msingi, ujenzi wa wodi ya akina mama na mtoto .
Fedha kiasi cha Shilingi Milioni 578.85 zilipokelewa kutoka kwa wadau wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa afua za Afya kupitia mfuko wa pamoja wa Afya, UNICEF, GAVI, Global fund, JHPIEGO, Lishe na ICAP.
Wakichangia taarifa hiyo katika Mkutano wa Mwaka, waheshimiwa Madiwani wakiongozwa na Mstahiki Meya Mhe. Renatus Mulunga .kwa pamoja wamemshukuru na kumpongeza. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi Ilemela kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali.
Sambamba na hilo wametoa pongezi kwa Mkurugenzi na timu ya wataalam kwa namna ambavyo wameshirikiana katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka lengo la mwaka 2022/2023 fedha ambazo zimetumika katika utekelezaji wa miradi katika kata zote 19, ambapo Mstahiki Meya alitumia fursa hiyo kuhimiza juu ya suala la ukusanyaji wa mapato kwa kasi ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi huku akiwataka Madiwani kuwaachia kazi ya kukusanya mapato wataalam ili kuweza kufikia lengo la bajeti ya mwaka 2023/2024
“Ili tuwe na maendeleo katika manispaa ya ilemela tukusanye mapato kwa kasi tusipokusanya mapato ya kutosha hatutaweza kuwahudumia wananchi, kazj ya halmashauri ni kutoa huduma na si vinginevyo”., Mhe Mulungu alisema
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.