Tunayo kila sababu ya kuipinga rushwa kwani ni adui wa haki imeingia kila mahali katika jamii yetu na kuleta matatizo makubwa ambayo hadi sasa yanatugharimu kurudisha hali nzuri ya kimaadili iliyokuwepo awali.
Hayo yamesemwa na mratibu wa kamati ya maadili mkoa wa Mwanza Mchungaji Robert Bundala wakati alipokuwa akichangia mada wakati wa kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya robo ya kwanza kwa mwaka fedha 2024/2025 ( Julai hadi Septemba) ya utekelezaji wa kamati ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) ya Wilaya ya Ilemela ambayo yeye kama kiongozi wa dini ni mjumbe.
".. Watoto wanabakwa na ndugu zao, familia zinanyamaza kwa kigezo cha kulinda heshima ya familia bila kujali madhara anayoyapata mtoto,matukio ya ulawiti yamekuwa mengi wahusika wanatoa rushwa kesi zinakosa muendelezo zinakufa.."
Mch.Bundala amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kupunguza ubize na kumrudia Mungu kwani matukio ya kikatili yanayoendelea ndani ya jamii yanahitaji hofu ya Mungu kukabiliana nayo .
Sarah Nthangu ni mratibu wa MTAKUWWA Ilemela amesema kuwa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 kamati hiyo imefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 8 ambao tayari mahakama imewatia hatiani kwa makosa ya ukatili wa kingono kwa watoto na wamepewa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Nae Askari wa dawati la jinsia Ilemela Bi.Leah Ogutu ameomba timu yao iwe inaalikwa kwenye vikao vya shule vinavyohusisha wazazi ili kupata nafasi ya kuzungumza nao na kutoa elimu kwa wote walimu, wazazi na wanafunzi ili kuleta uelewa wa pamoja.
Daniel Andrew na Jacinda Malele ni wawakilishi wa baraza la watoto Manispaa ya Ilemela wao wanasema ipo haja ya wanafunzi kuchanganyika katika program mbalimbali za kitaaluma kuanzia ukaaji darasani ili kuwaondolea mawazo hasi ya kutamaniana jinsia moja na kuwaomba wazazi kufika shuleni kufuatilia maendeleo ya kitaaluma na mienendo mingine ya maisha ya kawaida pindi mtoto anapokuwa shuleni na nje ya shule.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.