VIKUNDI VYATAKIWA KUZUNGUSHA FEDHA ZA RUZUKU
Vikundi vyote vinavyonufaika na fedha za ruzuku kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela vimetakiwa kuzungusha fedha hiyo katika shughuli mbalimbali za uzalishaji ili kukidhi malengo ya Serikali katika kutoa fedha hizo.
Hayo yamesemwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ukimwi ya Manispaa hiyo Mheshimiwa Shabaan Ramadhan Maganga wakati wa ziara ya kamati yake iliyohusisha ukaguzi wa huduma za upimaji na unasihi katika kituo cha afya Buzuruga na Shaloom Care House kabla ya kuhitimisha katika kikundi cha Ujasiriamali cha Upendo Pasiansi ikiwa ni ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa katika manispaa yake chini ya kamati ya Ukimwi kwa robo ya nne 2016/2017.
“Jitahidini sana angalau kila mtu apate pesa za mtaji msikubali kuweka pesa zote zikae tu benki bila sababu ya msingi wakati mzunguko wa mtaji wenu uko chini, Zungusheni pesa ili mkuze mitaji yenu mkifanya hivyo badala ya mtu kuwa na biashara moja atakuwa na biashara zaidi ya moja na sisi manispaa tupo pamoja nanyi lengo letu ni kuona fedha tunazowapa zinawasaidia kujikwamua kiuchumi”, Alisema.
Aidha Mhe Maganga ametaka kuchukuliwa hatua kwa vikundi vyote visivyofuata utaratibu sambamba na kuwa na matumizi mabovu ya fedha za ruzuku kwa lengo la kuhakikisha ruzuku hiyo inayotolewa inaenda kuwasaidia walengwa na si kunufaisha watu wachache wenye maslahi binafsi.
Nao wajumbe wa kamati hiyo wakichangia walisisitiza suala la kutolewa kwa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha ili kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha kwa vikundi hivyo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kikundi cha wajasiriamali Upendo Pasiansi Bi Martha Pius kwa niaba ya wenzake mbali na kuishukuru Manispaa ya Ilemela chini ya mwenyekiti wa kamati ya Ukimwi ameiomba Serikali kuona namna bora katika kuhakikisha inawaongezea ruzuku ili kuimarisha mtaji walionao ukilinganisha na uwezo wa uzalishaji wa kikundi chao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.