Mstahiki meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe. Renatus Mulunga amewataka watendaji kuweka nguvu katika suala la ukusanyaji wa mapato na kuwataka waheshimiwa madiwani kushirikiana na watendaji hao ili kuweza kufikisha lengo la ukusanyaji wa mapato.
Ameyasema hayo wakati akihitimisha kikao cha Baraza maalum ambalo limepokea na kujadili hesabu za mwisho za Halmashauri za mwaka wa fedha 2021/2022.
“Kuendesha halmashauri kunahitaji fedha hivyo watendaji hakikisheni mnaweka nguvu katika suala la ukusanyaji wa mapato na waheshimiwa madiwani niwatake kuunga mkono juhudi za watendaji katika suala zima la ukusanyaji wa mapato”, amesema Mhe Mulunga
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala akiwasilisha salam za serikali amelipongeza Baraza la Madiwani pamoja na timu ya wataalam chini ya Mkurugenzi wa Manispaa kwa namna Halmashauri inavyoendelea kupiga hatua katika kuwahudumia wananchi wa Ilemela.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunazitatua changamoto za wananchi ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema suala zima la ukusanyaji mapato sambamba na miradi ya maendeleo”. Amesema Mhe Masala
Nao waheshimiwa madiwani wa Manispaa ya Ilemela kwa nyakati tofauti wamempongeza Mkurugenzi na timu ya wataalam kwa namna ambavyo miradi ya maendeleo inatekelezwa katika kila kata, na kusema kuwa Ilemela inaendelea kupiga hatua kila mwaka ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Pamoja na hayo wamewataka watendaji kuhakikisha wanafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha kuwa Ilemela inaendelea kupata hati safi kama ilivyo kwa miaka mingine.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi, Mweka Hazina wa Manispaa ya Ilemela Ndugu Julius Ndyanabo amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kama ilivyo halmashauri zingine kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1982 kifungu Na. 40 (Pamoja na marekebisho yaliyofanyika mwaka 2000) imekamilisha ufungaji wa hesabu za mwisho na baadae kuziwasilisha kwa mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali(CAG)
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.