Vitabu 160 vya rejista za wakulima kwa ajili ya ruzuku ya mbolea vimetolewa kwa watendaji wa kata 19 za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa lengo la kupata takwimu sahihi na halisi za wakulima ili kuwezesha kusajiliwa katika mfumo rasmi kwa ajili ya kuja kupatiwa ruzuku ya mbolea hapo baadae.
Afisa Kilimo wa Manispaa ya Ilemela Bi.Neema Semwaiko akiwakabidhi vitabu hivyo amewataka watendaji wa kata kuwa makini katika zoezi la usajili wa wakulima wote waliopo ndani ya maeneo yao ili kurahisisha zoezi la ugawaji wa mbolea.
Aidha Bi.Semwaiko amewasisitiza kuwa kila mkulima ataandikishwa mahali shamba lake lilipo hata kama wamiliki wa shamba ni zaidi ya mmoja atasajiliwa mtu mmoja tu kwa niaba ya wengine lengo likiwa kurahisisha zoezi la ugawaji punde taratibu zote zitakapokamilika.
“Wakulima wote watapaswa kusajiliwa hata kama mkulima amekodi shamba,atasajiliwa kama mmiliki kwa wakati huo kwani ndiye anaelitumia kwa kipindi hicho.” Amesema Semwaiko
Mpango huu wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima unasimamiwa na mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mbolea ikiwemo tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI),serikali za mitaa,mabenki ya biashara na wafanyabiashara wa mbolea nchini.
Nae mtendaji wa kata ya Bugogwa ndugu Mkono ameipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kilimo na kuwapunguzia mzigo wananchi wake katika masuala mazima ya kilimo na kuahidi kuunga mkono jitihada zote za serikali za kuleta maendeleo kwa wananchi wake akiamini kuwa ruzuku hii italeta chachu na tija katika suala zima la mapinduzi ya kilimo Ilemela na Tanzania kwa ujumla.
Katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni150 kwa nchi nzima kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ili kupunguza makali ya bei ya mbolea kwa wakulima sambamba na kuongeza uzalishaji wenye tija katika kilimo na kuwezesha utekelezaji wa ajenda 10/30 ya “kilimo ni Biashara”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.