Watendaji wa kata na mitaa wa Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha masuala ya lishe kwenye kata na mitaa yao kwa kuhakikisha wanawahimiza wahudumu ngazi ya jamii kuwaibua watoto waliopo mitaani na kuwapeleka katika vituo vya huduma za afya ili kupata huduma bora na kuepusha vifo vya watoto.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Bi Mariam Msengi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Hassan Masala katika kikao cha tathmini ya lishe wilaya ya Ilemela kilichoketi tarehe 19 Julai 2023 kwa lengo la kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.
“Niwatake watendaji wa kata kuhakikisha mnakuwa mstari wa mbele katika suala la lishe ili kuhakikisha tunakuwa na jamii inayozingatia lishe bora” .Aliongeza Bi Msengi.
Aidha kupitia kikao hicho wajumbe walipitia taarifa ya kadi alama ya lishe ya mwaka 2022/2023 ambayo ilionekana kupanda ukilinganisha na mwaka 2021/2022 ambapo viashiria vingi vikiwa na asilimia kati ya 70-100 na hivyo kuwa katika rangi za kijani na njano ambapo rangi ya kijani inawakilisha vizuri na njano ikiwakilisha wastani iliyowasilishwa na Afisa Lishe, Bi Pili
Pamoja na mafanikio hayo yaliyobainishwa katika kadi alama ya lishe zipo changamoto mbalimbali zilizobainishwa ikiwemo suala la ushiriki mdogo wa wanaume katika mafunzo ya jiko darasa hivyo ikatolewa rai kwa watendaji wa kata na mitaa kuwaelimisha wanaume juu ya umuhimu wao katika kushiriki kwenye mafunzo hayo mara yanapotolewa katika mitaa yao ili kuweza kuimarisha afya za watoto kwani wanaume wengi ndio wanaotoa fedha za manunuzi ya chakula.
Kadhalika wajumbe walipata fursa ya kujadili juu ya zoezi la siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIKI) ambayo inalenga kuimarisha mifumo ya kijamii ya utoaji na usambazaji wa huduma endelevu za afya na lishe ya mama, mtoto na jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.