Watumishi wa makao makuu ya halmashauri ya manispaa ya Ilemela wametakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuwahudumia wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa divisheni ya utawala na rasilimali watu manispaa ya Ilemela Bi.Leokadia Humera wakati wa kikao kazi na watumishi Manispaa ya Ilemela ambacho kilikuwa na lengo la kuwakumbusha watumishi juu ya haki na wajibu wao katika utumishi wa umma sambamba na kusikiliza na kupokea kero zao kwa lengo la kuboresha utendaji kazi utakaoleta matokeo chanya.
Akiwasilisha mada kuhusu wajibu na haki ya mtumishi wa umma Bi. Humera amezitaja haki mbalimbali za mtumishi wa umma ikiwemo likizo ya mwaka kwa kila mtumishi,haki ya kustaafu na mafao stahiki, sambamba na haki ya kupata matibabu kwa mujibu wa kanuni na sheria za kazi kwa watumishi wa umma.
‘.. Ni muhimu watumishi wote wa umma kufahamu haki na wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwani wataweza kuepuka mambo yasiyofaa na kutenda yale yanayotakiwa kwa mlengo wa kutoa huduma bora kwa wananchi tunaowahudumia ..’
Aidha amefafanua kwa undani kanuni na sheria za kazi zinazomtaka mtumishi kutimiza wajibu wake kama kuwahi kazini, kuwepo kazini muda wote wa kazi na kuepuka utoro na kubainisha makosa mepesi na mazito na adhabu zake.
“Ni wajibu wa watumishi wote wa umma kufanya kazi kwa ushirikiano,upendo na kuepuka makundi yasiyofaa kwa lengo la kutoa huduma kwa wateja wetu na sisi wenyewe kuweza kuwajibika ipasavyo katika nafasi zetu kwa amani. “ amesema Bi. Humera.
Akihitimisha kikao hicho Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amesema ni wajibu wa kila mtumishi kutambua nafasi yake katika utendaji na kuahidi kuendelea kutoa nafasi ya vikao kama hivyo kwa watumishi wote wa Halmashauri kwa maslahi mapana ya ustawi wa manispaa ya Ilemela pamoja na kuahidi kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na watumishi hao katika kikao kazi hicho.
Mayala Nyanda ni mmoja wa watumishi waliohudhuria kikao hicho yeye anashukuru kwa utaratibu huu wa watumishi kupewa elimu juu ya wajibu na haki zao kwani utasaidia watumishi kutobweteka na kufanya kazi za viwango vinavyokubalika kila siku.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.